Mpaka sasa, hakuna ushahidi au uhakika wa asilimia 100 kwamba kuna maisha katika sayari nyingine, au hata miezi (moons).
Pamoja na hayo, kuna sababu za msingi ambazo zinanifanya kufikiri kwamba ni suala la muda tu kabla hatujagundua aina fulani ya maisha katika Sayari nyingine.
Zifuatazo ni sababu 7 zinazonifanya mimi na wanaSayansi wengine kuamini kwamba, hatupo peke yetu katika Ulimwengu:
1. Uwepo wa viumbe viishivyo katika mazingira magumu (Extremophiles) duniani:
Moja ya swali kubwa ambalo wengi hujiuliza ni: Je maisha yanaweza kustahimili katika mazingira ambayo ni tofauti kwa namna moja ama nyingine na Dunia?
Jibu linaonekana kuwa ni: NDIYO!
Hii ni kwasababu, hapa Duniani kwetu, kuna viumbe ambavyo vinaishi katika mazingira magumu, ambayo usingetegemea viumbe vyaweza kustahimili. Kuna viumbe vinaishi katika joto kali mno, vingine katika baridi kali mno, vingine hustahimili katika mazingira ambayo ni sumu kwetu kikemikali, cha ajabu: vingine huweza hata kustahimili kwenye uvurungu (vacuum).
Tumegundua viumbe ambavyo huweza kuishi bila oksijeni karibu na vent za volcano chini ya bahari. Viumbe kama "tardigrades" huishi katika vacuum.
Hivi pamoja na vingine vingi vinatudhihirishia msemo: "Maisha ni popote..." Na hii inanifanya mimi kuamini kwamba, hata katika Sayari nyingine ambapo mazingira yake ni tofauti kabisa na Dunia, maisha yanaweza yakastahimili.
2. Ushahidi wa "vianzilishi maisha" vya kikemikali katika Sayari nyingine na miezi (moons):
Kutokana na nadharia ambayo inatawala sasa katika ulimwengu wa Sayansi ni kwamba: Maisha katika dunia yametokana na myeyungano ya kikemikali (chemical reactions) ambayo ikatengengeneza membreni za seli (cellular membranes) na proto-DNA.
Myeyungano hii inaonekana kuanzishwa na "complex organic compounds" kama: nucleic acids, protini, carbohydrates na lipids ambazo zinapatikana katika anga pamoja na bahari.
Kuna ushahidi wa kutosha kwamba: "vianzilishi" hivi vipo pia katika sayari nyingine na miezi.
Mfano mzuri ni katika mwezi wa Saturn uitwao "Titan", wanaSayansi wamegundua vianzilishi hivi katika anga lake. Wamegundua pia uwepo mkubwa wa vianzilishi hivi katika nebula ya Orion.
Naomba kurudia kwamba: Hatujagundua maisha, lakini tumegundua viungo vinavyoaminika na wanaSayansi wengi kuwa vianzilishi vya maisha katika Dunia yetu. Kama viungo hivyo havipo tu Duniani bali pia katika sehemu nyingine, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na maisha katika Sayari nyingine na si tu Duniani.
3. Kukua kwa namba ya Sayari zinazofanana na Dunia:
Kwa miaka ya hivi karibuni, wanaSayansi wamegundua Sayari kadhaa ambazo kwa namna moja ama nyingine zinafanana na Dunia yetu... shida ni kwamba ziko mbali, hali inayofanya iwe ngumu kuzifuata na kuzichunguza kwa ukaribu zaidi kama tulivyofanya katika sayari ya Mars.
Sayari hizo zinafanana na Dunia yetu kwasababu zinazunguka nyota amabazo zinaendana kidogo na Jua letu... Nyota hizo ni kama: "Beta Canum Venaticorum", "HD 10307", "HD 211415", "18 Scorpii", "51 Pegasus", na nyingine nyingi....
4. Ukubwa, wingi na Utofauti wa maisha katika Dunia:
Si tu kwamba maisha yalianza Duniani katika mazingira magumu na kustahimili ukame, baridi, nyoto, volcano na hata sumu; Maisha hayo yameweza kumea na kuneemeka kiasi kwamba kuna aina tofauti tofauti za viumbe.
Hali hii inanifanya nihisi kuna aina nyingine tena za maisha katika Sayari nyingine.
5. Utata juu ya namna Maisha yalivyoanza Duniani:
Pamoja na kwamba kuna nadharia mbalimbali juu ya namna maisha yalivyoanza kama ile niliyoitaja katika pointi yangu ya pili, bado kuna utata na hatuna uhakika wa asilimia mia juu ya namna maisha yalivyoanza Duniani.
Kadiri tunavyojifunza zaidi kuhusu Dunia na mazingira yake, nadharia mbalimbali zinazidi kuibuka.
Nadharia moja common ni ile inaitwa "Panspermia", Nadharia hii inadai: Maisha yaliyoanza Duniani ni yale ya seli moja (single-celled life) lakini chimbuko lake ni kutoka Sayari nyingine pengine Mars, na yalifika Duniani kwa njia ya kimondo (meteorite)...
6. Ushahidi wa kukua kwamba kuna Bahari na maziwa (Lakes) katika Sayari nyingine:
Pamoja na nadharia kadhaa, Tuna ushahidi mkubwa, na wa kutosha kwamba maisha yalianzia kutoka Baharini.
Na sasa vilevile tuna ushahidi mkubwa na wa kutosha kwamba hapo awali kulikuwa na Maji katika sayari ya Mars, na hata Titan (mwezi wa Saturn). Mwezi wa Jupiter vilevile ambao unaitwa Europa, nao una bahari pia...
Kwa hali hiyo, kuna uwezekano pia kwamba maisha yapo, au yalikuwepo katika Sayari na miezi hiyo.
7. Nadharia ya Mageuko ya Spishi (Evolutionary Theory):
Nadhari hii inayotokana na Darwin inaonesha namna ambavyo maisha hupambana ili kuweza kustahimili mazingira yake...
Kwangu mimi, inanitumia ujumbe kwamba, ili kuwa na maisha katika sayari, tunachohitaji ni seli moja tu... na sidhani kama hilo ni jambo gumu...
Basi hizo ndizo sababu zangu kuu na za msingi kuamini kwamba kuna Maisha katika Sayari nyingine. Je! Una mawazo au fikra tofauti? Niambie mawazo yako yakiamabatana na sababu zako kufikiri hivyo... Una sababu zaidi kuamini kuna maisha katika Sayari nyingine, Naomba niambie! Una swali kuhusiana na sababu zangu, niulize bila woga...
SABABU 7 ZINAZONIFANYA KUFIKIRI KUNA MAISHA KATIKA SAYARI NYINGINE...
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment